Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (Jakaya Kikwete Cardiac Institute - JKCI) kinara utalii wa matibabu (Medical Tourism) Kusini mwa Afrika katika kuimarisha ushirikiano wa Kitaasisi katika kutoa huduma za matibabu bobezi ya moyo. Tarehe 11-18 Mei, 2024, Dkt. Angela Muhozya kutoka JKCI, Tanzania aliambatana na timu ya madaktari bingwa 19 kati yao 16 kutoka Marekani na wengine watatu kutoka Denmark, Canada na India katika kambi maalum ya utoaji wa huduma ya matibabu na mafunzo ya moyo nchini Zambia kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa ya Moyo ya Zambia (National Heart Institute- NHH).
Alipofika Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Zambia kutoa taarifa fupi ya mafanikio makubwa ya JKCI kikanda na kimataifa, Dkt. Angela alikiri kuwa JKCI kutambuliwa kikanda na kimataifa kama Kituo Mahiri katika matibabu ya magonjwa ya moyo pamoja na tafiti ni matunda ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mpango endelevu wa kuwaendeleza Wataalamu wa Afya katika ngazi za ubingwa na ubobezi pamoja na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya upasuaji na matibabu ya moyo.
Kwa upande wake, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Zambia, Mhe Lt Gen Mathew Edward Mkingule aliipongeza JKCI kwa kutekeleza kwa vitendo dhima ya Taasisi hiyo na kueleza kuwa Jamhuri ya Zambia inashukuru uwepo wa ushirikiano wa Kitaasisi baina ya NHH na JKCI kutokana na mafanikio wanayoyapata katika kufanikisha upasuaji salama kwa wagonjwa wa moyo ambao wamepatiwa matibabu ya kibingwa. Balozi Lt Gen Mkingule alifurahi kuona hatua za ushirikiano zimeimarika hadi ngazi za kimataifa ambapo JKCI iliongoza jopo la madaktari bingwa 19 kutoka Marekani, Denmark, Canada na India katika utoaji wa mafunzo ya vitendo katika Hospitali ya Taifa ya Moyo ya Zambia na kufanikiwa kufanya upasuaji kwa wagonjwa wengi zaidi. Hii ni mara ya pili JKCI kuweka kambi ya matibabu nchini Zambia kwa mwaka huu 2024, kambi ya kwanza ilikuwa mwezi Januari 2024 ambapo wagonjwa wa moyo zaidi ya 9 walifanikiwa kufanyiwa upasuaji chini ya uongozi wa timu ya Wataalam kutoka JKCI kwa ushirikiano na Wataalamu wa NHH.