Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Zambia umeadhimisha miaka mitatu ya Siku ya Kiswahili Duniani ambayo huadhimishwa tarehe 7 ya kila mwaka kwa kuzindua darasa la kufundishia Lugha ya Kiswahili kupitia ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Zambia.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa darasa hilo ambao umefanyika hivi karibuni katika Chuo Kikuu cha Zambia, Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Lt. Jenerali Mathew Mkingule amesema kuwa uzinduzi huo ni hatua muhimu si tu katika kukuza lugha adhimu ya Kiswahili lakini pia katika kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Zambia.
Aidha, katika kuhamasisha na kuchagiza mwamko wa kujifunza lugha ya Kiswahili nchini Zambia, Mhe. Balozi Mathew alitumia fursa hiyo kutangaza ufadhili wa nafasi 6 zitakazotolewa na Ubalozi kwa wanafunzi wa Kiswahili kwa ngazi ya awali ambapo kati hizo nafasi mbili (2) zitatolewa kwa Wizara ya Elimu, nafasi mbili (2) kwa Shirika la Utangazaji la Zambia na zilizosalia zitatolewa kwa Idara ya Habari Maelezo ya Zambia (ZANIS).
Pia wageni waalikwa kwenye hafla hiyo walipata nafasi ya kusikiliza ujumbe wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kuhusu umuhimu wa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani na mchango wa Tanzania katika kuanzishwa siku hiyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Bw. Jeol Kamoko ambaye alimwakilisha mgeni rasmi Waziri wa Elimu wa Zambia Mhe. Douglas Syakalima (Mb) kwenye hafla hiyo alisema Serikali ya Zambia itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu kupitia lugha ya kiswahili ili kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.
Kadhalika, ilielezwa kuwa, kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia kwa kushirikiana na wadau wa Kiswahili nchini wakiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Serikali ya Zambia imepata mwamko na kuonesha shauku kubwa ya kufundisha Lugha ya Kiswahili kwa kuanzia na mafunzo ya muda mfupi katika ngazi tatu ya awali, kati na mwisho.