Balozi Mathew Edward Mkingule amepongeza Timu ya Madaktari na Wauuguzi kutoka  Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (Jakaya Kikwete Cardiac Institute - JKCI) kwa kuendelea kutoa huduma za kibobezi za matibabu na upasuaji wa moyo katika Jamhuri ya Zambia. Timu hiyo ya Madaktari bingwa na Wauguzi kutoka JKCI walifika nchini Zambia na kushirikiana na Wataalam wa Hospitali ya Taifa ya Moyo ya Zambia katika kufanya upasuaji na kutoa matibabu kwa watoto wenye matatizo ya moyo waliokuwa wamelazwa katika Hospitali hiyo. Huduma hizo za upasuaji zilianza kutolewa kuanzia tarehe 23 hadi 28 Septemba, 2024.

Baada ya Timu hiyo kufika Ubalozi na kutoa taarifa fupi ya ujio wao nchini Zambia. Balozi Mkingule aliishukuru Timu hiyo ya Madaktari Bingwa na Wauguzi kutoka JKCI  kwa kutumia taaluma zao katika kuokoa maisha ya watoto waliofanyiwa upasuaji kwa mafanikio. Alieleza kuwa Ubalozi utaendelea kushirikiana na JKCI katika kufanikisha azma yake ya kuwa Taasisi Mahiri ya Matibabu ya Moyo Barani Afrika pamoja na kushirikiana na Taasisi za Nchi rafiki katika tafiti na matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa wa moyo. 

Balozi Mkingule alitoa ahadi ya Ubalozi kuendelea kutangaza huduma zinazotolewa na JKCI na kueleza kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya afya nchini na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi mahiri wa  Rais wa JMT Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan  ni ukombozi si tu kwa afya za Watanzania bali na Wananchi wa Mataifa jirani na Mataifa mengine nje ya Afrika. JKCI imeendelea kuwa kinara katika kutoa huduma bora na za teknolojia ya hali ya juu na kwa gharama rafiki. Kufuatia mafanikio hayo, Balozi Mkingule ametoa wito kwa Hospitali kubwa za Tanzania (Muhimbili, Benjamin Mkapa, MOI, Ocean Road na nyinginezo )kujitangaza kimataifa na kuanzisha mashirikiano yatakayosaidia kuongeza ubora wa huduma wanazozitoa.